Habari

Watumishi jiji la Arusha watakiwa kudumisha upendo na kufanya kazi kwa bidii

Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia akizungumza na wafanyakazi wa jiji la Aruhs wakati alipokwenda kuwaaga.
    Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia akizungumza na wafanyakazi wa jiji la Aruhs wakati alipokwenda kuwaaga.

Watendaji na Watumishi wa Serikali katika jiji la Arusha wametakiwa kushirikiana,kupendana na kufanya kazi kwa bidii ili kulinda mafanikio ya kimaendeleo yaliyofikiwa na jiji hilo.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Arusha na aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt. Athumani Kihamia wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi jijini hapo.

Akizungumza na Watumishi na Watendaji wa jiji hilo Dkt. Kihamia amewataka wafanye kazi kwa bidii na kuepuka vitendo vinavyoweza kuleta mgawanyiko miongoni mwao.

Amesema katika kipindi cha uongozi wake akiwa Mkurugenzi wa jiji hilo aliwaunganisha watumishi wote akiweka msisitizo katika bidii, nidhamu ya kazi na matumizi mazuri ya rasilimali na fedha Serikali hali iliyolifanya jiji hilo kupata Hati Safi ya Matumizi ya fedha za Serikali.

“Watumishi Wenzangu mimi nimekaa katika jiji hili kwa muda wa miaka 2, nafurahi kuwa nawaacha mkiwa na morali ya kufanya kazi na muendelee kufanya kazi kwa bidii, mzidi kupendana ili kazi mnazozifanya zifanikiwe kwa manufaa ya jiji ” Amesisitiza Dkt. Kihamia.

Ameongeza kuwa ili jiji hilo liendelee kupiga hatua zaidi za Kimaendeleo, watendaji na wakuu wa Idara wana wajibu wa kufanya kazi kwa pamoja, kuaminiana na kuepuka kufanya vitendo vya dhuruma na uonevu wa aina yoyote kwa watumishi wa kada mbalimbali walio chini yao.

Amesema maendeleo yaliyofikiwa katika jiji hilo yasingekuwepo kama watumishi waliopo wasingekuwa waaminifu na wanaoshauri vizuri na kuwataka wakuu wa Idara, watendaji na watumishi wanaotoa maamuzi kuepuka vitendo vinavyoweza kushusha chini morali ya kazi ya watumishi.

“Watendaji mlio na mamlaka msifanye mabadiliko yoyote kwa kumwonea mtu, mafanikio haya tusingeweza kuyapata kama kusingekuwa na watumishi wanaofanya kazi zao kwa bidii na uaminifu wapo watumishi walio na utendaji mzuri na wanaoshauri vizuri hawa tuendelee kuwalinda na kuwaheshimu” Amesisitiza Dkt.Kihamia.

Katika hatua nyingi Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia amesema kuwa maandalizi ya Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Udiwani utakaofanyika Agosti 12 mwaka huu yanaendelea na vizuri katika maeneo mbalimbali yenye uchaguzi huo.

Amesema kuwa mpaka sasa hakuna changamoto zozote kubwa za kiutendaji zinazoweza kukwamisha uchaguzi huo.

“ Mchakato wa uchaguzi unaenda vizuri, mpaka sasa hakuna kasoro zozote na zoezi la Kampeni linakwenda vizuri hakuna vurugu wala vitendo vya uvunjifu wa amani vilivyoripotiwa mpaka sasa kutokana na kampeni hizo” Amesema Dkt. Kihamia.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa jiji hilo Mhe. Karisti Lazaro akizungumza na Watendaji na watumishi wa jiji hilo waliohudhuria kwenye hafla hiyo amempongeza Dkt. Athumani Kihamia kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)

Ameeleza kuwa uteuzi wake umezingatia viwango vyake vya utendaji kazi uliotukuka katika jiji hilo la Arusha uliolenga kuleta maendeleo kwa wananchi.

“ Nichukukue fursa hii kumpongeza sana kwa namna ambavyo Mhe. Rais amemuona katikati ya majiji yote kwa kuona anafaa kumsaidia katika majukumu makubwa ya kitaifa”

Amewaeleza watumishi hao kwamba wana kila sababu ya kujifunza kutoka kwa Dkt. Kihamia kwa kuwa yeye alitimiza wajibu wake kwa uaminifu mkubwa na kuongeza kuwa kuwa kutokana na utendaji wake jiji la Arusha liko katika hali nzuri ya mapato kwa kuwa na asilimia zaidi ya 103, uanzishaji wa miradi mikubwa ya Afya, Elimu, Maji na Usafirishaji ambayo yote inalenda kuinua uchumi wa jiji la Arusha.

“Hili ni fundisho kwetu, Mkurugenzi unayeondoka umetuachia jiji letu likiwa salama, tuko kwenye mazingira mazuri sana, leo unaiacha Halmashauri ikiwa na mapato kwa zaidi ya asilimia 103 ikiwa na Hati safi na hoja chache sana maana ulipoingia ulikuta hoja 400 za CAG leo unaondoka ikiwa na hoja 23 ambazo zote zinajibika, hii yote inatokana na udhibiti wake” Amesisitiza Mhe. Lazaro.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa jiji hilo Afisa Mtendaji wa Kata ya Ngarenaro Bw. Braison Nassari ameeleza kuwa wao kama watumishi wa jiji hilo wanamwelezea Dkt. Athumani Kihamia kama Mkurugenzi aliyekuwa akiwatunza watumishi wa Serikali katika jiji hilo.

Amesema kwa kipindi chote alichokuwa Mkurugenzi Dkt. Kihamia hakukubali kuyumbishwa na mtu yeyote wakiwemo wanasiasa waliopingana naye katika hatua zake alizozichukua katika kusimamia taratibu za Serikali na utumishi wa umma.

“ Napenda kuweka wazi kwamba sisi kama watumishi wa jiji la Arusha tunakupongeza sana, kwa kipindi chote ulichokuwepo hapa tuliona kwamba hata watu walipokuwa wakileta maneno ya hila wewe ulichukua hatua ya kuchunguza mambo hayo, na hata baadhi ya watu waliotaka kukutengenezea mambo mengi ya kukuchafua hawakuweza kufanikiwa ulisimamia katika kulinda haki, ukweli na taratibu za utumishi “ Amesisitiza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *