Habari

Wagombea 30 wa udiwani wapita bila kupingwa uchaguzi mdogo wa udiwani

Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia
                                                                     Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia

Wagombea 30 wa udiwani katika uchaguzi wa kata 77 wamepita bila kupingwa, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt. Athumani Kihamia amesema.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam jana, Dkt. Kihamia amesema kwamba madiwani wote waliopita bila kupingwa wanatoka Chama cha Mapindizi (CCM).

“Katika Uchaguzi huu wa Kata 77 Wagombea Udiwani katika Kata thelathini (30) wamepita bila kupingwa na wagombea hao wote ni wa Chama cha Mapinduzi (CCM),” alisema.

Dkt. Kihamia amefafanua kwamba wagombea hao wamepita bila kupingwa baada ya Tume kukutana, kujadili na kuyatolea maamuzi mapingamizi mbalimbali yaliyoweka na wagombea wa udiwani.

Amesema kwamba rufaa zilipokelewa na kujadiliwa kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 44(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kikisomwa pamoja na Kanuni ya 28(1)(2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2015.

“Tume, ilipokea, ilijadili na kufanya maamuzi ya Rufaa 25 ambapo jumla ya wagombea kumi (10) walifanikiwa na hivyo kuendelea na uchaguzi na wagombea 15 rufaa zao hazikufanikiwa na hivyo kutoendelea kuwa wagombea,” alisema.

Dkt. Kihamia amesema kwamba katika kata sabini na saba (77) wanachama 254 kutoka vyama kumi na moja (11) vya siasa walichukua fomu za uteuzi na kwamba jumla ya wanachama 186 sawa na asilimia 73.2 ya waliochukua fomu za uteuzi walizirejesha na kuteuliwa kuwa wagombea ambapo kati yao wagombea 179 sawa na asilimia 96.2 ni wanaume na wagombea 7 sawa na asilimia 3.8 ni wanawake.

“Hadi muda wa mwisho wa uteuzi ulipofika (saa 10.00 jioni siku ya uteuzi) wanachama 68 sawa na asilimia 26.8 ya waliochukua fomu hawakuteuliwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kutorudisha fomu, kurudisha fomu nje ya muda unaokubalika kisheria na fomu kutojazwa ipasavyo,” alisema.

Dkt. Kihamia amesema katika uchaguzi huu mdogo wa madiwani jumla ya vyama kumi na moja (11) vimesimamisha aagombea.

Wagombea katika Kata kwa kila Chama ni kama ifuatavyo: ACT-Wazalendo Wagombea 17 (sawa na asilimia 22), ADC Wagombea 3 (sawa na asilimia 3.9), CCM Wagombea 77 (sawa na asilimia 100) CHADEMA Wagombea 54 (sawa na asilimia 70), CHAUMMA Wagombea 2 (sawa na asilimia 2.6), CUF Wagombea 17 (sawa na asilimia 22), Demokrasia Makini Wagombea 4 (sawa na asilimia 5.2), NCCR-MAGEUZI Wagombea 6 (sawa na asilimia 8), NRA Wagombea 3 (sawa na asilimia 3.9), SAU Mgombea 1 (sawa na asilimia 1) na UPDP Wagombea 2 (sawa na asilimia 2.6).

Wakati huohuo, Dkt. Kihamia amesema kwamba katika jimbo la Buyungu jumla ya wanachama kumi (10) kutoka vyama kumi (10) vya siasa vya AAFP, ACT-Wazalendo, CCM, CHADEMA, CUF, DP, Demokrasia Makini, NRA, UMD na UPDP walichukua fomu za uteuzi.

“Wanachama wote kutoka vyama hivyo walirejesha fomu na kuteuliwa kuwa wagombea wa Ubunge katika Jimbo hilo, kati yao wanaume ni tisa (9) na mwanamke mmoja (1),” amesema Dkt. Kihamia.

Amevitaka vyama vya siasa na wagombea wao kuzingatia maadili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015, wakati wote wa kampeni na siku ya uchaguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *