Habari

Tume yawataka viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao wajitokeze kujiandikisha au kuboresha taarifa zao

Viongozi wa Dini wakimsikiliza Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao juu ya kushiriki kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura au kuboresha taarifa zao ili kila mwananchi mwenye sifa za kuandkishwa akaandikishwe na yule anayeboresha taarifa zake akaboreshe.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage wakati akifungua mkutano wa Tume na viongozi wa dini jijini Dar es Salaam leo, ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura ambayo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Jaji Kaijage amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatambua umuhimu wa viongozi wa dini na iwapo viongozi hao wakielewa vyema mchakato wa uandikishaji na uchaguzi kwa ujumla watawawezesha wananchi kushiriki katika mchakato wa uchaguzi kwa amani kwani wanaongoza kundi kubwa la wananchi na wanao ushawishi mkubwa kwa waumini wao.

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amesema taasisi yake inatambua umuhimu wa viongozi wa dini na imekuwa ikiwatumia viongozi hao kuhamasisha ushiriki katika chaguzi kwa amani na kutokana na juhudi za viongozi hao, chaguzi hizo zimekuwa zikifanyika kwa amani na utulivu.

Akijibu baadhi ya maswali ya viongozi hao wa dini, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia amesisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itandelea kutenda haki katika kusimamia chaguzi na kuendelea kukutana na wadau wa uchaguzi na kuwapa elimu ili kupunguza malalamiko yanayotolewa katika chaguzi.

Dkt. Kihamia amewaeleza viongozi wa dini kuwa kwa sasa malalamiko katika chaguzi mbalimbali yamepungua kwa kiwango kikubwa na amewahakikishia kuwa yataendele kupungua.

Wakizungumza kwenye mkutano huo, baadhi ya viongozi wa dini wameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwashirikisha katika mkutano huo kwani wanaamini viongozi wa dini wakishirikishwa ipasavyo kwenye mchakato wa uchaguzi, chaguzi zitaendelea kufanyika kwa amani na mafanikio.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kukutana na wadau wa uchaguzi ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura unaotarajiwa kuanza Julai mwkaa huu ambapo Jumanne ya wiki itakutana na wawakilishi wa taasisi za wanawake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *