Habari

Tume yatangaza Uchaguzi Mdogo Jimbo la Buyungu na Kata 79 za Tanzania Bara

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo katika Jimbo la Buyungu, Mkoani Kigoma na kwenye Kata 79 za Tanzania Bara.

Akitangaza kufanyika kwa uchaguzi huo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji (R), Semistocles Kaijage amesema kuwa uchaguzi huo utafanyika Agosti 12 mwaka huu na fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kuanzia tarehe 8 hadi 14 mwenzi huu (Julai).

“Uteuziwa Wagombea utafanyika tarehe 14 Julai, mwaka huu. Kampeni za Uchaguzi zitafanyika kati ya tarehe 15 Julai, hadi tarehe 11 Agosti, mwaka huu na siku ya uchaguzi itakuwa ni tarehe 12 Agosti mwaka huu,” amesema Jaji Kaijage.

Jaji Kaijage amebainisha kuwa Tume imetangaza uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge kwenye Jimbo la Buyungu baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mhe. Ndugu Job Ndugai juu ya uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika jimbo hilo.

Amesisitiza kuwa Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, aliitarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya Mbunge wa Jimbo la Buyungu katika Halmashauri ya Kakonko Mkoani Kigoma kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Kasuku Samson Bilago.

Kwa upande wa nafasi wazi za Udiwani Jaji Kaijage amesema kuwa Tume ilipokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana akiitaarifu juu ya uwepo wa nafasi wazi za Udiwani katika Kata 79.

“Tume imepokea Taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaaa mbaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, aliitarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata 79 za Tanzania Bara,” amesisitiza Jaji Kaijage.

Ametoa wito kwa vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi cha Uchaguzi mdogo.

Jaji Kaijage amefafanua kuwa kuwa uchaguzi huo mdogo utafanyika ndani ya Halmashauri 43 zilizopo kwenye Mikoa 24 ya Tanzania Bara.

Mikoa hiyo ni pamoja na, Kigoma, Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Katavi, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Mtwara, Morogoro, Mwanza, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida, Songwe, TaboranaTanga.

Kwa upande wa Halmashauri zitakazokuwa na Uchaguzi ni Moshi, Ruangwa, Mbulu, Hanang, Babati, Serengeti, Tarime, Kyela, Mtwara, Newala, Kilombero, Kilosa, Kwimba, Makete, Wanging’ombe, Kalambo, Songea, Msalala, Meatu, Singida, Songwe, Tunduma, Tabora, Nzega, Urambo naTanga.

Halmashauri nyingine ni pamoja na Karatu, Longido, Arusha, Ngorongoro, Monduli, Meru, Ubungo, Kondoa, Mpwapwa, Chamwino, Iringa, Kyerwa, Misenyi, Muleba, Nsimbo, Kasulu na Same.Orodha ya kata 79 inapatikana kwenye Tovuti ya Tume kwa anuani ya www.nec.go.tz.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *