Habari

Tume kushirikisha wadau kila hatua kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage akisoma hotuba ya ufunguzi wa mkutano kati ya Tume na viongozi wa vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam Machi 05, 2019.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage akisoma hotuba ya ufunguzi wa mkutano kati ya Tume na viongozi wa vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam Machi 05, 2019.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesisitiza kuwa itashirikisha wadau wa uchaguzi hususan Vyama vya Siasa katika kila hatua inayopitia kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao wa Mwaka 2020.

Aidha kwa kuanzia Tume imeanza kupitia na kufanya marekebisho katika kanuni za Uchaguzi kwa kuhuisha na kuboresha kanuni zilizoandali8wa chini ya sharia ya Taifa ya Uchaguzi na ile ya Serikali za Mitaa za mwaka 2008.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage wakati akifungua rasmi mkutano wa Tume na Vyama vya Siasa uliofanyika jijini Dsm kwa lengo la kuwafahamisha kuhusu marekebisho yalivyofanywa, sababu za marekebisho pamoja na kupokea maoni na ushauri kutoka Vyama vya Siasa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kushiriki kwa Vyama vya Siasa katika katika hatua hizo za mwanzo kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuzielewa Kanuni hizo ni sehemu ya kufanikisha zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Mheshimiwa Kaijage ametaja maandalizi mengine yaliyofanywa kuwa ni pamoja na uhakiki wa vituo vya kuandikisha Wapiga Kura, vifaa vya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na uboreshaji wa Mkakati wa Elimu ya Mpiga Kura.

Akifafanua kuhusu uhakiki wa vituo vya kuandikishia Wapiga Kura Kaijage amesema vimeongezeka kutoka 36, 549 vilivyotumika mwaka 2015 hadi vituo 37, 407. Aidha vituo 6,208 vimebadilishwa majina na vituo 817 vimehamishwa kutoka Kijiji/Mtaa mmoja kwenda mwingine huku vituo 19 vikihamishwa kutoka Kata moja kwenda nyingine.

Aidha kwa upande wa Zanzibar Mwenyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amesema uhakiki umeonyesha kuwa vituo vimeongezeka kutoka 380 hadi kufikia vituo 407.

Kuhusu vifaa kwa ajili ya Uboreshaji wa Daftari Mheshimiwa Kaijage amesema mchakato wa kupata vifaa kwa ajili ya ukarabati wa BVR kits umekamilika na kwamba kinachosubiriwa ni kuvifanyia majaribio ya Uandikishaji.

Majaribio ya Uandikishaji na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unatarajiwa kufanyika katikia Kata mbili za, Kihonda katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Kibuta iliyopo nkatika Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.

Akiwasilisha mada kuhusu maboresho ya Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mkutano huo Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Dkt Athumani Kihamia amesema lengo la kuvishirikisha Vyama vya Siasa ni kujenga misingi ya demokrasia inayolenga kuendesha chaguzi huru, wazi na za kuaminika.

Mkutano huo wa Tume na Vyama vya Siasa umehudhuriwa pia na Msajili nwa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi pamoja na viongozi mbalimbali wa Vyama vya Siasa vilivyo na usajili wa kudumu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *